Nape na wenzie waonywa CCM


HATIMAYE Chama Cha Mpainduzi (CCM), kimeamua kufunguka na kutoa onyo kuhusiana na kauli za baadhi ya makada wake walioenguliwa na Rais John Magufuli katika nafasi mbalimbali za uongozi walizokuwa wakishikilia serikalini kabla ya kuenguliwa. 

Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga, ndiye aliyetoa onyo hilo linaloashiria kuwagusa makada wa chama hicho waliowahi kuteuliwa na Rais Magufuli kushika nafasi mbalimbali serikalini kabla ya kuenguliwa, akiwamo Nape Nnauye aliyeondolewa hivi karibuni kutoka katika nafasi ya kuwa Waziri wa Habari,

Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dk. Harrison Mwakyembe aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba ndiye aliyeteuliwa kushika nafasi ya Nape huku mteule mpya wa Rais Magufuli kwa nafasi iliyoachwa na Mwakyembe Wizara ya Sheria akiwa ni Prof. Palamagamba Kabudi.

Lubinga hakutaja jina la kiongozi yeyote aliyekumbwa na mkasa huo, lakini miongoni mwa makada walioenguliwa katika nafasi zao hivi karibuni ni Nape ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi.

Baada ya kuenguliwa, Nape alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na baadaye na wananchi wa jimbo lake, akielezea kuridhia uamuzi wa Rais Magufuli huku akisisitiza kuwa sasa anaelekeza nguvu zake jimboni kwa nia ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Nape aliwahi pia kueleza kuwa yeye hakugombea kuwa waziri bali ubunge kwa tiketi ya chama chake (CCM) ili kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo lake, lakini akimshukuru pia Magufuli kwa kumuamini katika uwaziri kwa takribani mwaka mmoja.

Akizungumza mjini Iringa juzi, katika mkutano na wanafunzi wa vyuo vikuu vilivyopo mkoani humo ambao ni wanachama wa CCM na pia viongozi wa chama hicho wa matawi na kata,
Lubinga aliwataka makada walioteuliwa na Rais na kisha kuondolewa katika nafasi walizopewa kuacha kupiga kelele au kulalamika, bali wakubali mabadiliko kwa nia ya kuheshimu busara za Ikulu kwa maamuzi yaliyofanywa dhidi yao.

“Rais anapoteua viongozi wake kuwapa dhamana anaona kwamba wewe anakuhitaji katika nafasi hiyo na mazingira yaliyopo yanakuhitaji kwa wakati huo…lakini inapofika wakati anakuondoa, ujue kwamba mazingira yale huwezi kuyamudu na anakuokoa ili usipate laana,” alisema Lubinga na kuongeza:

“Busara za Ikulu ziheshimiwe na zisijadiliwe, kwamba mimi sijapata... ni kwa sababu baadhi ya viongozi wameondolewa madarakani, lakini wamebaki wakilalamika mitaani ovyo.”

Lubinga alisema hivi sasa, CCM imejipanga zaidi kimkakati kuhakikisha kuwa inajenga nidhamu na uwajibikaji ndani ya serikali iliyoingia madarakani kwa tiketi yake kupitia uchaguzi mkuu uliopita.

MIKAKATI ZAIDI CCM

Katika hatua nyingine, Lubinga alisema jambo jingine linalopewa kipaumbele na CCM kwa sasa ni kuwaondoa watendaji wote ambao huonekana kuwa kikwazo katika utekelezaji wa mipango ya serikali ya kujenga uchumi imara kupitia sekta ya viwanda na uzalishaji.

Kwa sababu hiyo, Lubinga alisema CCM wakati inafanya mabadiliko, ilichukua hatua ya kuona wapi inakwama na nani anakwamisha, hasa kwa kula rushwa au kwa kuwa wanafiki.
Katika hatua nyingine alisema kuwa waliosababisha jimbo la Iringa kupotea sio wananchi wapigakura bali ni viongozi wake.

Kuhusiana na kushindwa kwa CCM kutwaa Jimbo la Iringa katika uchaguzi mkuu uliopita, Lubinga alisema wameshajua kuwa tatizo ni viongozi wao wenyewe na siyo wananchi, hivyo sasa wanajiimarisha kwa kuondoa kasoro zilizokuwapo awali ili jambo hilo lisijitokeze tena.

“Iringa mmeona viongozi wa juu walitupa matatizo… kiukweli waliosababisha kupoteza jimbo la Iringa siyo wananchi wapigakura bali ni viongozi ndiyo waliofanya mkalipoteza,” alisema Lubinga na kuongeza: “Sasa jengeni Iringa Mpya.”

Akizungumza katika mkutano huo, Katibu wa Jumuiya ya Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Iringa, Abdulkarim Halamga, aliwataka wana-CCM kuwa waadilifu na kushiriki katika kukijenga upya chama chao.

Hivi karibuni, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu, alifukuzwa uanachama akiwa ni miongoni mwa makada waliokutwa na hatia mbalimbali, wengine wakiwa ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT), Sophia Simba, na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida.

Wenyeviti wengine wa mikoa waliovuliwa uanachama wa CCM ni Christopher Sanya (Mara) na Erasto Kwilasa (Shinyanga).


EmoticonEmoticon